Wednesday, 2 April 2014

MH BURA: UBUNGE WA VITI MAALUM UFUTWE

 Mjumbe wa Bunge la Katiba, Felister Bura amependekeza Katiba inayotungwa ifute Ubunge wa Viti Maalumu.

Amesema kuwa kuwa ubunge wa viti maalumu umekuwa hauna faida zaidi ya udhalilishaji ambao wamekuwa wakiupata kutoka kwa watu wengine.
Bura alitoa kauli hiyo alipokuwa akichangia kwenye Semina ya Wajumbe wa Bunge la Katiba ambayo iliandaliwa na Chama cha Wabunge Wanawake (TWPG) na kufanyika kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa.
Bura ni mbunge wa viti maalumu katika Bunge la Muungano akiwakilisha Mkoa wa Dodoma na tayari amedumu katika Bunge hilo kwa vipindi vitatu.

“Nafasi hii ya ubunge wa viti maalumu inakera na inatia aibu. Tunadhalilika sana sisi wabunge wa viti maalumu kwani tunatukanwa kila kona tunayopita,” alisema Bura.
Alisema mwaka 2010 alisimama mwanamke mwingine katika jengo la Ubungo Plaza na kuwatukana wabunge wa viti maalumu kwamba wanapata nafasi hizo baada ya kutoa rushwa ya ngono.
Mbunge huyo alisema kuwa kumekuwa na hali ya kuwafanya wanawake wa Tanzania kuwa nyuma kwa kila kitu licha ya kuwa idadi yao ni kubwa kuliko wanaume na kuwa wakiamua wanawake kushika dola.
Alitoa mfano kuwa katika nchi ya Malaysia kuna wilaya ambayo kwa asilimia 80 inaongozwa na wanawake kwa sababu waliamua na wakaweza kufaya hivyo.
Pendekezo la mjumbe huyo ni kutaka Katiba impe nafasi Msajili wa Vyama vya Siasa kuwalazimisha wanasiasa kuingiza wanawake katika nafasi tatu za juu kuliko ilivyo sasa nafasi zote zimeshikiliwa na wanaume


.

No comments:

Post a Comment